This post is also available in: 简体中文 (Chinese (Simplified)) English (English) Français (French) Español (Spanish) Português (Portuguese, Portugal) Română (Romanian) Filipino (Filipino) Deutsch (German)
Majibu ya kiislamu juu ya uovu na mateso
Tumesikia swali hili mara nyingi: ‘‘Kwanini mambo mabaya yanatutokea sisi au watu tuwapendao?’’ Hakika sisi sote tumeathiriwa na hali ngumu katika maisha kwa njia moja au nyingine. Kila mmoja wetu amewahi kupata huzuni, iwe kutokana na mambo yaliyomkuta yeye au kwa kusikia maumivu ya mtu mwingine. Matukio huwa hayaishi.
Mateso ya binadamu na maovu, yameenea na yapo kweli. Hizi ni nguvu katika hii dunia. Sasa tutakabiliana nayo vipi?
Baadhi ya watu wanakabiliana nayo kwa kumkasirikia Mwenyezi Mungu au kwa kukataa kwamba Mwenyezi Mungu mwenye upendo anaweza kuwepo wakati uovu umejaa duniani. Tatizo la kufikiria hivi ni kwamba uovu na maumivu yanayotukumba yanaendelea kutusababishia maumivu na hakuna kinachobadilika baada ya kumlaumu Mwenyezi Mungu au kuukataa uwepo wake. Kwa hiyo tutakubalina vipi na hili kiukweli?
Jibu katika Uislamu
Uislamu una jibu lilonaweza kutusaidia kukabiliana na maumivu yetu katika njia inayoridisha.
Quran inatumia visa na simulizi nzuri kubadilisha dhana yetu juu ya uovu na maumivu. Fikiria kwa mfano, kisa cha mtume Musa na mtu aliyekutana nae kwenye safari aitwaye Khidhr:
“Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa rehema kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu.
Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule uwongofu ulio funzwa wewe?
Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami.
Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani wake?
Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako.
Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi nianze kukutajia.
Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi (yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika umefanya jambo baya. Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?
(Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau, wala usinipe uzito kwa jambo langu.
Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana, akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama hakika umefanya jambo baya kabisa! AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami? Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu.
Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya.
(Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia. Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote. Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri. Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma. Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria”. [1] Quran Surah Al- Kahf (sura ya 18) aya ya 65-82.
Kisa hichi pia kinatupa mafunzo muhimu na ufahamu wa kiimani. Somo la kwanza ni kwamba ili kuelewa mpango wa Mwenyezi mungu, itabidi mtu awe mnyenyekevu. Mtume Musa ana hadhi kubwa kiimani katika Quran, na ndiye mtu aliyetajwa zaidi katika Quran, hata hivyo alimuendea khidhr kwa unyenyekevu. Mtume Musa alijua kwamba Khidhr alipewa elimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo yeye (Musa) hakuwa nayo. Musa aliomba kwa unyenyekevu kujifunza kutoka kwake, lakini khidhr alimjibu kwa kumuuliza juu ya uwezo wake wa kuwa mvumilivu; hata hivyo Musa alisisitiza kwamba alitaka kujifunza.
Somo la pili ni kwamba uvumilivu unahitajika ili kuweza kuhimili maumivu na uovu, kiimani na kisaikolojia katika dunia hii. Khidhr alijua Musa asingeweza kumvumilia, kwa kuwa atafanya vitu ambavyo Musa ataviona kama ni vitu viouvu. Musa alijaribu kuwa mvumilivu lakini alishuku kwa kuuliza matendo ya mtu huyu na alionyesha hasira yake alipohisi uovu umetendeka. Hata hivyo, mwisho wa kisa hichi, Khidhr alielezea hekima kutoka kwa Mungu iliyomfanya afanye matendo, haya baada ya kuelezea kwamba Musa hakuweza kuwa mvumilivu.
Somo jingine ni kwamba hekima ya Mwenyezi Mungu haina mwisho na ni kamili, wakati hekima na elimu yetu sisi ina mipaka. Njia nyingine ya kuelezea hili ni kwamba Mwenyezi Mungu ana hekima na elimu kamili; tuna sehemu ndogo tu, yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye mwenye picha kamili, sisi tuna kipande tu. Tunaona vitu kutokana na muono wetu unaotokana na ujuzi wetu ulio vipande vipande. Aya isemayo “Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani wake?” ina maanisha kuna hekima ya Mwenyezi Mungu ambayo hatuwezi kuifikia. Khidhr alikuwa na elimu juu ya hekima ya Mwenyezi Mungu na faida zilizojificha ambazo Musa hakuweza kuziona.
Kuna mifano mingi maishani mwetu inayotufanya tukiri juu ya udhaifu wetu kiakili. Tunakubali mambo yanayotutokea mara kwa mara ambayo hatuwezi kuyaelewa. Kwa mfano, tunapoenda kwa daktari tunadhani kwamba daktari ana mamlaka. Ndio maana tunaamini uaguzi wake. Tunakunywa dawa anazotuandikia pia bila kuwa na shaka.
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye hekima, na majina na sifa zake ni kamilifu, kuna busara kwenye kila afanyalo, hata kama hatujui wala hatuelewi busara yake. Wengi wetu hatuelewi jinsi magonjwa yanavyojitokeza lakini kwa sababu tu hatuelewi kitu hakuwezi kupinga uwepo wake.
Kisa cha Musa na Khidhr pia kinahusiana na hoja ya zamani ya kumpinga Mwenyezi Mungu. Hoja hiyo ni: kama Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu kuliko wote na ndiye mwingi wa rehema, hivyo basi hakutakiwi kuwe na uovu duniani. Kwa kuwa yeye ndiye mwenye nguvu kuliko wote, Mwenyezi Mungu angesitisha uovu wote duniani lakini uovu bado upo, hivyo basi aidha Mwenyezi Mungu sio Mwenye rehema kiasi hicho kwa kuwa anaachia uovu uendelee au hana nguvu kiasi hicho kwa kuwa hawezi kuusitisha uovu huo.
Hoja hii inaweka dhana ya Mwenyezi Mungu aliye Mwingi wa rehema na mwenye nguvu katika hali ngumu. Hakika sifa hizi sio sifa pekee za Mwenyezi Mungu, yeye pia ndiye mwingi wa busara na mjuzi wa yote, ana busara ambayo sisi hatuna kama ilivyo kwene kisa kilichoelelezewa. Hoja iliyowekwa hapo juu itafanya kazi kama Mwenyezi Mungu angekuwa na sifa mbili tu, Mwenye nguvu na Mwenye rehema, lakini hii sio kweli kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye busara na mjuzi wa yote pia, hivyo tatizo hili halipo tena.
Lengo letu ni ibada
Lengo kuu la maisha katika Uislamu sio kufurahia furaha ipitayo; ila ni kupata utulivu wa moyo kwa kumjua na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Ibada ni istilahi pana katika Uislamu, jambo lolote jema tunalofanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni ibada, iwe kutafakari juu ya viumbe, kutoka sadaka, kufunga, kutabasamu, kutafuta matibabu au kufikiria mema juu ya Mwenyezi Mungu na kusamehe makosa ya watu, vyote hivi huchukuliwa kama ibada kama vikifanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Kutekelezwa kwa lengo hili kutasabibisha amani ya milele na furaha ya kweli. Kwahiyo kama hili ndilo lengo letu kuu, basi vipengele vingine vya uzoefu katika maisha ya binadamu vitafuata tu, baada ya lengo hili kuu.
Fikiria mtu ambaye hajawahi kupitia mateso yoyote au maumivu, lakini hupata furaha muda wote. Mtu huyu, kutokana na raha aliyonayo, atamsahau Mwenyezi Mungu na hivyo atakuwa ameshindwa kutimiza lengo aliloumbiwa. Mlinganishe mtu huyu na yule anayepitia shida na maumivu ambayo yanamfanya amuelekee Mwenyezi Mungu na kutekeleza lengo lake maishani. Kulingana na mtizamo wa imani ya Kiislamu, yule ambaye maumivu yake yamemuelekeza kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yule ambaye hajawahi kupata maumivu na raha yake imemfanya awe mbali na Mwenyezi Mungu.
Maisha ni mtihani
Mwenyezi Mungu ametuumba kwa ajili ya kutupa mtihani, na sehemu ya mtihani huu ni kupata majaribu kwa kupitia maumivu na uovu. Kufaulu mtihani huu kutatuwezesha kupata makazi ya kudumu yenye furaha ya kudumu peponi. Quran inaeleza kwamba Mwenyezi Mungu ameumba maisha na kifo, “ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha”. Quran sura ya 67 aya ya 2
Katika hali ya kawaida, wasiomuamini Mwenyezi Mungu hawajaelewa lengo la uwepo wetu duniani. Dunia inatakiwa kuwa uwanja wa majaribu na dhiki ili kupima matendo yetu ili tuweze kupata uchamungu. Kwa mfano, tunawezaje kupata uvumilivu wakati hatujawahi kuwa kwenye hali zitazoujaribu uvumilivu wetu? Tutapataje ujasiri bila hatari ya kuikabili? Tutakuwaje wenye huruma kama hakuna anayehitaji kuhurumiwa? Maisha kuwa mtihani kuna jibu maswali haya. Tunahitaji vitu hivi ili kuhakikisha ukuwaji wetu wa kitabia na kiroho. Hatupo hapa kwa ajili ya kuwa na raha muda wote; hilo ni lengo la pepo.
Hivyo basi, kwanini maisha ni mtihani? Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ana wema ulio kamili, anataka kila mmoja wetu aamini na mwishowe kupata furaha ya milele pamoja naye peponi. Mwenyezi Mungu anaweka wazi kwamba anapendelea wote tuwe na imani: “lakini hafurahii kufuru kwa waja wake.” Quran sura ya 39 aya ya 7
Hii inaonyesha wazi kwamba Mwenyezi Mungu hataki yeyote aende motoni. Hata hivyo, angeamua kumpeleka kila mtu peponi, kungekuwa hakuna uadilifu; Mwenyezi Mungu angekuwa anaweka usawa kati ya Hitler na Yesu. Mfumo unahitajika ili kuhakikisha kwamba watu wanaoingia peponi wanaingia kwa kustahili. Hii inaelezea kwanini maisha ni mtihani. Maisha ni mfumo tu wakuona nani miongoni mwetu anastahili furaha ya milele. Ndio maana, maisha yamejaa vikwazo, vinavyopima matendo yetu. Hivyo, Uislamu unawezesha kwa kuwa unaona mateso, uovu, madhara, maumivu na matatizo kama mtihani.
Uzuri wa Uislamu ni kwamba Mwenyezi Mungu, anayetujua zaidi ya tunavyojijua, ameshatuwezesha na kutuambia kwamba tuna uwezo wa kuyakabili majaribu haya. “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo”. Quran sura ya pili aya 286
Hata hivyo, tukishindwa kuyakabili majaribu haya baada ya kujaribu kadri ya uwezo wetu, rehema ya Mwenyezi Mungu na uadilifu wake utahakikisha tutalipwa kwa njia moja au nyingine, aidha katika maisha haya au katika maisha yafuatayo yanayotusubiri.
Kufarikiana na dunia
Katika Uislamu Mwenyezi Mungu ametuumba ili tumuabudu na tumkaribie yeye. Kanuni ya msingi kuhusu hili ni kwamba ni lazima tufarikiane na hali ya mapito ya dunia hii. Dunia hii ni sehemu yenye vizuizi, maumivu, uharibifu, tamaa, ubinafsi, anasa na uovu. Kuteseka kunaonyesha jinsi maisha haya yalivyo duni, hivyo kutusaidia kufarikiana nayo. Na hivyo ndivyo tunavyoweza kumkaribia Mwenyezi Mungu.
Mtume Muhammad (saw) alisema: “Kuipenda dunia ndio chanzo cha uovu wote.” uovu mkubwa zaidi katika Uislamu ni kumkataa Mwenyezi Mungu na kumhusisha na miungu wengine.; hivyo ni lazima kufarikiana na dunia hii ili kufikia lengo la kiimani la kumkaribia Mwenyezi Mungu, na hivyo kuipata pepo.
Quran inaweka wazi kwamba dunia hii ni starehe ya kupumbaza: “Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua”. Quran aya ya 57 aya ya 20
‘Tatizo’ la uovu na mateso sio tatizo kwa waumini, kwa kuwa uovu na mateso vinaeleweka kama sehemu ya busara ya Mwenyezi Mungu, ukamilifu na wema wake. Mafunzo ya kiimani ya Uislamu yanaunda hisia za matumaini, uvumilivu na utulivu. Maana ya kimantiki ya kutomuamini Mwenyezi Mungu ni kwamba mtu anakuwa katika hali ya kukata tamaa na hakutokuwa na majibu juu ya kwanini uovu na mateso yapo. Kutokujua huku ni kutokana na ubinafsi unaowafanya washindwe kutazama mambo kwa mtizamo mwingine.
Marejeo
[1] Aya kutoka Suratul Kahf (surah ya 18) ya Quran – Aya ya 65-82