This post is also available in: English (English) Español (Spanish) Português (Portuguese, Portugal) Română (Romanian) Filipino (Filipino) Deutsch (German)
Ushawahi kuwaza upendo ni nini kiuhalisia? Hebu fikiria kidogo kuhusu hili.
Sio rahisi kufafanua. Mshairi mmoja aliwahi kuandika kwamba pindi kalamu itapowekwa kwenye karatasi na ikaandika kuhusu upendo, basi inakatika vipande viwili. Tukijaribu kuelezea upendo wetu, tunapata tabu sana kupata maneno sahihi. Kauli tunazotumia haziwakilishi kikamilifu hisia zinazowaka katika sakafu za mioyo yetu. Hii inaweza kuelezea kwanini tunahusisha upendo na matendo na sio tu maneno.
Tunakumbatiana, tunawanunulia zawadi tuwapendao na kuwabusu watoto wetu. Hakika upendo ni hisia yenye nguvu, ya kipekee na isiyoweza kuepukika.Tunavipenda vitu au watu kwa sababu wanatufanya tujiskie vizuri. Watu wengi wanawapenda watu kutokana na yale waliyowafanyia. Kwa mfano; watu wanawapenda wazazi wao kutokana na yale waliowafanyia. Walitujali, walitulea na kutupatia mahitaji yetu. Hii husababiha hisia za shukurani na upendo.
Kutokana na hili, tunaona kwamba kwa upande mmoja, upendo bila shaka, unatokana na hisia za shukrani za dhati. Ni hisia hii inayotufanya tutake kurudisha na kulipiza wema. Pia tunaweza kumpenda mtu sio kwa sababu ametufanyia jambo lolote ila jinsi tu walivyo, inatufanya tuwapende.
Mfano wa watu hawa ni mashujaa katika historia. Hata kama hatufaidiki moja kwa moja na waliyoyafanya, tabia zao kama ujasiri, ukarimu na ubunifu unatufanya tuwapende.
Kumpenda Mwenyezi Mungu
Inahuzunisha kwamba unaweza kumpenda mtu ambaye hakupendi tena au mtu ambaye hakuwahi kukupenda katu.
Jambo hili linaweza kukuumiza sana na kukusumbua. Lakini kuna upendo wa aina moja tu ambao haupo hivyo. Upendo mbao hakika ni wa aina yake; huo ni upendo wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka tuutafute upendo wake. Kwa wale watakaoianza safari hio, hakika Mwenyezi Mungu anawapenda pia.
Hakika unaweza kuwa mtu anayependwa na Mwenyezi mungu, na ishara ya upendo huo ni kwamba unasoma ujumbe huu sasa hivi! Moja katika majina ya Mwenyezi Mungu ni ‘Mwingi wa Upendo’. Yeye ndiye chanzo cha upendo wote. Upendo wake ni mkubwa kuliko upendo wowote wa kidunia tuliowahi kuushuhudia.
Jambo hili linatakiwa litufanye tuutake upendo wake kwa dhati kwa kuwa hii ndio zawadi kubwa zaidi ambayo mtu yeyote anaweza kupewa. Upedo wa Mwenyezi Mungu ni chanzo cha utulivu wa kiroho, amani na utulivu wa milele katika maisha yajao.
“Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!” Qur’an Sura ya 13 aya ya 28
Upendo wa Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko upendo mwingine wa aina yoyote; ukiwemo upendo wa mama. Upendo wa mama, hata kama ni wakujitolea, unatokana na haja yake ya mpenda mtoto wake. Unamkamilisha, na kwa kupitia kujitolea kwake, anahisi ukamilifu na kuridhika. Lakini tunapouzungumzia upendo wa Mwenyezi Mungu, yeye hamtegemei mtu yeyote na anajitosheleza mwenyewe na ni mkamlifu. Hahitaji chochote, wala upendo wake hautokani na kuhitaji au kutaka kitu chochote; hivyo basi ni aina ya upendo ulio wa dhati kuliko wote.
“Mwenyezi Mungu anampenda mja wake kuliko mama anavyompenda mwanawe”
Mtume Muhammad (SAW)
Njia ya kuuelekea upendo
Mwenyezi Mungu ndiye anayependa zaidi kuliko viumbe wote na anataka kukupenda wewe kwa upendo wake maalumu
Lakini ili kuweza kuupokea upendo huo kikamilifu, na ili upendo huo uweze kuleta maana, itabidi umpende yeye na ufuate njia ielekeayo kwenye upendo wake. Upendo unawasilishwa kwa vitendo; anayekupenda atakuonyesha upendo wake. Alama dhahiri kwamba unampenda Mwenyezi Mungu ni kumfanya yeye ndiye pekee unayemuabudu. Katika Uislamu, ibada ni istilahi pana inayomaanisha kumfahamu Mwenyezi Mungu, kumpenda Mwenyezi Mungu, kumtii na kufanya mambo yote kwa ajili yake yeye peke yake. Jambo lolote zuri tunaloweza kulifanya linaweza kuwa ibada; au kumtukuza Mwenyezi Mungu, kuwafanyia wema wazazi na familia, kutafakari juu ya mazingira, kutoa sadaka, kufunga, kutabasamu, kutafuta tiba au hata kuwa na mawazo mazuri juu ya Mwenyezi Mungu na kusamehe makosa ya watu. Yote haya yanazingatiwa kuwa ni ibada, kama yatafanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
“Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia. Na katika watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana.”
Qur’an sura ya 2 aya 163-165
Kuujua upana wa ukarimu na upendo wa Mwenyezi Mungu utatufanya waja wenye shukrani. Upendo unatokana na shukrani, na hupelekea tuwe karibu na Mwenyezi Mungu. Yeye pia anakuwa karibu na sisi. Utahisi uwepo wa rehema yake na msamaha wake, utashuhudia uhalisia wa upendo wake kwa sababu ukimkumbuka Mwenyezi Mungu yeye pia hukukumbuka. Hivyo basi mja anampenda Mola wake na Mola wake anampenda yeye.
“Mwenyezi Mungu aliyejuu amesema; nipo jinsi mja wangu anavyonidhania nilivyo. Nipo nae atakaponitaja. Akinitaja nafsini mwake basi na mimi nitamtaja nafsini mwangu; akinitaja kwenye umati, nitamtaja kwenye umati mkubwa zaidi yake. Akinikurubia urefu wa kiganja ntamkurubia urefu wa mkono. Akinijia kwa kutembea ntamuendea nikikimbia.” Mtume Muhammad (saw)
Katika Uislamu, kumuabudu Mwenyezi Mungu kunamaanisha pia kukubali kwamba hamna chochote kinachochangia katika ubunifu, nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na kwamba tunayakinisha kwamba majina yake na sifa zake ni vyake peke yake. Sifa njema zote anastahiki yeye na yeye pekee ndiye wakuombwa pale tunapohitaji msaada.
“Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu, Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo. Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. Tuongoe njia iliyo nyooka, Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea.” Qur’an sura ya 1 aya ya 2-7
Majina na sifa za Mwenyezi Mungu hazina upungufu wala dosari. Hana watoto wa kiume wala wa kike. Hakuzaliwa wala hatafariki katu. Ni wa kipekee na hafanani na chochote katika viumbe vyake au chochote tunachoweza kufkiria; hana mipaka na ndiye mkamilifu kwa kiwango cha hali ya juu kuliko vyote.
Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee. Mwenyezi Mungu Mkusudiwa. Hakuzaa wala hakuzaliwa. Wala hana anaye fanana naye hata mmoja.
Qur’an sura ya 112 aya ya 1-4
Ishara ya Upendo
Ishara ya upendo wetu ni kwa yale tuyatendayo. Kumpenda Mwenyezi Mungu sio tu kauli; ni kwa kuthibitisha na hudhihirishwa kwa yale tunayoyafanya na watu tunaobadilika kuwa.
Kumuabudu Mwenyezi Mungu ndio njia kubwa kuliko zote za kuonyesha upendo wetu kwake. Kuna sababu tatu ambazo itabidi zimshawishi mtu yeyote mwenye akili timamu kumuabudu Mola wake kwa moyo wake wote, roho yake, nguvu na akili.
Asili ya Mwenyezi Mungu
Mungu, kiistilahi, ni yule ambaye anastahili ibada zetu; ni ukweli ambao una ulazima katika uwepo wake. Muda wote tunawasifia watu kutokana na ubora wa sifa zao, hata kama hawatunufaishi moja kwa moja kwa chochote. Hebu zingatia tunavyowashangilia na kuwapenda wanamichezo, wasanii na wanasayansi. Lakini, majina na sifa za Mwenyezi Mungu zimekamilika, wala sio kama binaadamu. Hii inamaanisha kwamba Mwenyezi Mungu anastahili kusifiwa kwa hali ya juu kuliko watu wote. Mwenyezi Mungu ndiye anayatakiwa atustaajabishe na ukubwa wake uyanyakuwe mawazo yetu.
Tunajifunza zaidi juu ya asili yake ya kipekee kwa kutizama mazingira; aina mbalimbali za viumbe ardhini, baharini na angani vyote ameviumba yeye. Ulimwengu wote huu mpana ni sehemu ndogo tu ya viumbe vyake vyote!
“Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana. Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.”
Qur’an sura ya 35 aya ya 27-28
Nyanja muhimu kuhusu kumuabudu Mwenyezi Mungu ni kwamba ni haki yake kuabudiwa, hata kama sisi sio wapokezi wa faraja yeyote. Kumuabudu Mwenyezi Mungu sio kama biashara kwamba anatupa neema na sisi tunamuabudu kama malipo. La hasha! Anaabudiwa kutokana na yeye alivyo na sio kwa jinsi sisi tunavyoamua kuzisifu neema zake.
“Mwenyezi Mungu – hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele.”
Qur’an sura ya 2, aya ya 255
Neema za Mwenyezi Mungu
Kama tukilifikiria hili kwa kina, itabidi tumshukuru Mwenyezi Mungu milele kwa sababu hatuwezi kumshukuru vya kutosha kwa neema zake zote ambazo ametupa. Kila kitu tulichonacho katika maisha yetu, kila kitu tunachokipenda kwa dhati, kinatoka kwake; kutoka kwenye uwezo wetu wa kupumua mpaka wale tunaowapenda ambao ametuumbia katika maisha yetu. Fikiria tu moja ya neema hizi; moyo wa binadamu.
Moyo wa binadamu unapiga takribani mara 100,000 kwa siku. Kila pigo la moyo ni la thamani kwetu. Yeyote miongoni mwetu anaweza akatoa kafara ya mlima wa dhahabu ili tu kuhakikisha kwamba mioyo yetu inafanya kazi vizuri ili kutuwezesha kuwa hai. Hakika lazima tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kila pigo linalotuwezesha kuwa hai. Kutokana na mtizamo huu, kingine chochote zaidi ya mapigo ya moyo ni nyongeza. Fikiria ni shukrani za aina gani inabidi tumpe kwa neema nyingine zote alizotujaalia.
Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
Qur’an sura ya 16 aya ya 78
Utegemezi wetu kwake
Mwenyezi Mungu ameumba kila kitu. Yeye ndiye mtoaji anayeutosheleza ulimwengu mzima na kuturuzuku kutoka kwenye fadhila zake. Qur’an inairudia dhana hii mara nyingi katika njia mbalimbali, ambazo zinaamsha hisia za kustaajabishwa katika moyo wa msomaji:
“Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa”
Qur’an sura ya 35 aya ya 15
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametuumba, uwepo wetu wenyewe unamtegemea yeye katika nyanja zote. Hatuwezi kujitegemea, hata kama baadhi yetu wamepotoshwa na wanadhani kwamba tunaweza. Hata kama tunaishi maisha ya starehe na urahisi au maisha ya umaskini na shida, mwishowe wote tunamtegemea Mwenyezi Mungu.Hakuna kitu ulimwenguni kinachowezekana bila yeye na chochote kinachotokea ni kutokana na idhini yake.
Hata mafanikio yetu katika biashara au vitu vikubwa tunavyoweza kuvifanikisha, vyote hivi ni kwa sababu ya Mwenyezi Mungu. Ameviumba vyanzo katika huu ulimwengu tunavyovitumia kupata mafanikio, na asiporuhusu mafanikio yetu hayawezi kutokea.
Kuelewa kwamba lazima tutafika mahali tutamtegemea tu Mwenyezi Mungu, inabidii kuamshe hisia za dhati za shukrani na unyenyekevu ndani ya mioyo yetu. Kumyenyekea Mwenyezi Mugu na kumshukuru ni njia ya ibada.
“Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?” Quran Sura ya 35 aya ya 3
Kukutana na Mpendwa wetu
Upendo wa Mwenyezi Mungu ni msingi muhimu katika uislamu.Ndio msingi wa kipekee katika yote anayoyafanya Muislamu.
Upendo wa Mwenyezi Mungu hauwezi kuelezewa kikamilifu wala kuhojiwa. Upendo ni jambo la moyo, sio akili. Maisha ni mafupi sana, usipoteze muda kupotoshwa na vitu vingine badala ya kutafuata mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu mwishoni mwa maisha yetu tutakutana na Mwenyezi Mungu huku akitupenda, kwa kuwa tulimuamini na kumfuata au akituchukia kwa sababu hatukumuamini na hatukuifuata njia yake.
“Yeyote atakayependa kukutana na Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu napenda kuktana nae na yeyote nayechukia kukutana na Mwenyezi Mungu, mweneyzi Mungu annachukia kukutana nae” Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake)
Hebu tuinyenyekeze mioyo yetu na tuombe muongozo wa Mwenyezi Mungu kwa dhati. Hakika hii njia ya kuulekea upendo wake na mafanikio ya milele. Mwenyezi Mungu mwenyewe anasema kwamba yeye ndiye mwingi wa rehema na atawafunika kwa upendo wake wale wanaoamini, wanaomuabudu na kufanya mema.
“Hakika walio amini na wakatenda mema Arrahmani Mwingi wa Rehema atawajaalia mapenzi”. Qur’an sura ya 19 aya ya 96.
Wale wanaoufuata mwongozo wa Mwenyezi Mungu kiuaminifu tu ndio wanastahili upendo wake. Hii inaeleweka vizuri kabisa. Mwenyezi Mungu hampendi mtu kutokana na utajiri wake, uzuri, ukoo, nguvu, ufasaha, akili, taifa lake wala jinsia. Ila Mwenyezi Mungu anawapenda wale ambao wanauhisi uwepo wake.
Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.
Qur’an sura ya 3 aya ya 31
Mwenyezi Mungu ametuonyesha njia ya kuupata upendo wake; kuifuata njia ya Mitume na wajumbe wake,ambao amewatuma katika vizazi vya binaadamu. Wote waliwaita watu wawe na uhusiano huo na Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwao ni Adamu, Nuhu, Ibrahimu, Musa, Isa (Yesu) na mtume wa mwisho Muhmmad (rehema na amani ziwe juu yake). Wao ni miongozo yetu katika kumpenda Allah.
Waislamu wanampenda Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) kwa sababu ameonyesha jinsi ya kuhusiana na Mwenyezi Mungu. Ujumbe wake ulikuwa rahisi: Mpende Mwenyezi Mungu kuliko kitu chochote na muabudu yeye peke yake, fuata muongozo wake na fanya mema. Hivyo basi kama unataka kukutana na Mwenyezi mungu, itabidi uupangiilie moyo wako kwamba usiwe na kitu chochote maishani mwako kilicho muhimu zaidi kuliko yeye. Kuna mtu aliwahi kumuliza mtume (rehma na amani ziwe juu yake) kuhusu siku ya kiyama. Hii ni siku ambayo Mwenyezi Mungu atahukumu nani ataingia peponi na nani anaingia motoni, kutokana na matendo yao.
Mtu huyo aliuliza “Kiyama kitakuwa lini?” Mtume akasema “umeandaa nini kwa ajili yake?” Mtu huyo akasema “Sijaandaa chochote isipokuwa ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake”. Mtume akasema: “Utakuwa na yule umpendaye”
Mtume Muhammad (rehema na Amani ziwe juu yake)
Muombe Mwenyezi Mungu muongozo, hakika Mwenyezi Mungu humuongoza yule atakae mwongozo kwa dhati na anayetamani kumuelekea yeye..