This post is also available in: 简体中文 (Chinese (Simplified)) English (English) Español (Spanish) Português (Portuguese, Portugal) Română (Romanian) Filipino (Filipino) Deutsch (German)
“Samahani nina kazi nyingi, sina muda!” kauli hii ni miongoni mwa majibu tunayoyasikia sana siku hizi na hakika ni ukweli.
Muda ni rasilimali yenye kikomo na tuna kila haki ya kuwa waangalifu juu ya jinsi tunavyoitumia kwa kuwa haiwezi kurejea! Tunauthamini muda pale tu tunapojua unakaribia kuisha. Masaa matano kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha kazi ndio yana mafanikio kuliko wiki tano zilizopita! Kwa kuwa muda una thamani, inakubidi ujue kwanini ujisumbue kusoma kitabu hichi.
Hivyo tunawasilisha jambo muhimu kuliko yote. Katika historia ya binadamu, Mwenyezi Mungu ametuma wajumbe wa kutuongoza. Lakini sasa, hilo limekwisha. Hakuna wajumbe tena. Wa mwisho ameshakuja na hakuna atakayekuja baada yake. Hakika mwisho umekaribia. Hivyo itakubidi uamue kama utauchukua ujumbe huu kwa mazingatio kwa kuwa hilo ndilo litabainisha mahali utakapoishi milele.
Hii haihusu imani ya upofu. Hakika huyu mjumbe alikuja na ushahidi ulio wazi uliounga mkono madai yake. Katika dakika chache zifuatazo, utajifunza kitu muhimu kuhusu mtu aitwae Muhammad.
Alidai kuwa yeye alikuwa mjumbe wa mwisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ndio, haya ni madai makubwa, lakini kuna kanuni tunayoweza kuitumia kujua kama madai haya ni ya kweli. Tukiacha mbali ubaguzi na tukiyatizama maisha yake kwa kina, kuna uwezekano madai yake yangekuwa kutokana na mambo matatu tu:
-Alikuwa muongo
-Alikuwa amechanganyikiwa
-Alikuwa anasema ukweli
Hakika kipimo hichi kinaweza kutumiwa kwa mtu anayeleta madai yoyote! Tutayachunguza madai ya Muhammad kwa kutumia kanuni hii.
Je, alikuwa muongo?
Kuitizama kidogo tu historia ya Muhammad ambayo imeandikwa kwa mapana kunadhihirisha ubora wa tabia yake. Alizaliwa katika mji wa Makka, katika kabila la kuheshimika la Bani Hashim ambao walikuwa wasimamizi wa njumba takatifu ya Mwenyezi Mungu, Kaaba. Hii ilikuwa miongoni mwa sababu ya Muhammad kujulikana na wengi. Jamii ya Kiarabu ya kipagani ilikuwa ya kikabila sana.
Hata hivyo, watu wa Makka walimuamini Muhammad kwa pamoja na wakampa cheo cha “Al Ameen”, kikimaanisha “anayeaminika”. Alijulikana sana kwa ukweli wake katika biashara na mahusiano yake na watu pamoja na kuwasaidia maskini, mayatima, wajane, wazee na walioonewa.
Uarabuni hapakuwa tu kuna ubaguzi wa kikabila, ila pia imani ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu ya Kiibrahimu ilikuwa imechafuliwa sana kwa kuabudu masanamu na imani potofu. Kuabudu masanamu ndio ulikuwa msingi wa mfumo wao wa kiuchumi, ujamaa na kisiasa. Alipofikia makamo ya miaka 40, Muhammad alianza kufundisha kwamba haya masanamu na imani potofu zinazoambatana nao, yalikuwa ya uongo na kwamba wanaoyaamini watapata adhabu ya milele kwa sababu ya kukiuka umoja wa Mwenyezi Mungu pekee aliye wa kweli.
Alikuwa muwazi katika kuwapinga juu ya dini zao za uongo. Sasa hebu fikiria. Kwanini afanye hivi kama alikuwa muongo? Watu waongo hudanganya ili kuepuka maumivu au kupata faida. Matendo haya ya Muhammad yanashabihiana vipi na hilo? Hakika wapagani walikuwa makini sana juu ya dini yao kwa kuwa iliwaunganisha na mababu zao na walijivunia kuwafuata. Ila Muhammad aliwaambia kwamba mababu zao (pamoja na mababu zake) walikuwa wamepotea na hawajui kitu.
Ndani ya muda mfupi Muhammad alitoka kuwa mtu aliyeheshimiwa na sasa kuwa mtu aliyechukiwa na kupingwa na viongozi wa Makka. Kwanza walijaribu kumpa rushwa. Walimpendekezea kumpa pesa, wanawake na hata ufalme ili tu aache ujumbe wake. Waliposhindwa wakamvamia, wakamtukana na kumpiga na hata kupanga njama za kumuua. Lakini badala ya kuacha ujumbe wake, alipaza sauti na kuendelea kuwapinga zaidi.
Wafuasi wake walikuwa wachache, lakini wao pia walipitia mateso na ilibidi wakimbilie nchi nyingine. Mwishowe yeye mwenyewe ilibidi aondoke nyumbani kwake na atafute makazi katika mji mwingine.
Kama angekuwa muongo na mdanganyifu aliyetaka kupata faida kutoka kwa watu, basi, kila mwanasiasa anajua kwamba, angeweza kukubaliana na matakwa ya watu na sio kuwapinga wazi wazi. Kwanini hakukubali mapendekezo yao walipomtaka aache ujumbe wake na achukuwe uongozi na utajiri? Labda wanaweza kudai kwamba motisha ya Muhammad kudanganya haikuwa kwa ajili ya ‘sasa na hapa’ lakini alitaka kuacha urithi wa kimawazo ili aweze kukumbukwa baada ya kufa kwake. Mpango wa ubatili wa kuendelea! Mtu anaweza kuleta madai haya tu kwa kutizama kutoka mwisho wa simulizi hii. Katika muda ule, kutizama kwa mtizamo wa nyenzo, Muhammad hakuwa na fursa ya kufanikiwa.
Kufanikiwa kwake kwenyewe ni jambo la kimiujiza. Zaidi, Muhammad alikuwa mnyenyekevu. Alihusisha mafanikio yake yote na Mwenyezi Mungu. Alivaa na kuishi kama watu wengine, licha ya uwezo wake wa kuweza kupata mali, yeye na familia yake waliishi maisha ya kawaida sana. Kama umaarufu ungekuwa ndio lengo lake, basi angedai kuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu na pia kuwaruhusu watu kuabudu masanamu yao.
Hakika wapagani waliamini uwepo wa Mwenyezi Mungu asiyeonekana ambaye ni muumba, na walichukulia masanamu yao kuwa waombezi wao kwa Mwenyezi Mungu. Kuwaita watu wamuabudu Mungu mmoja haikuwa njia ya kuchukua ili kupata umaarufu na nguvu (uongozi). Hakika, Muhammad aliwaonya watu kutokana na kumtukuza sana.
“Msinitukuze sana kama wakristo walivyomtukuza Mwana wa Mariamu (Yesu) kwa kuwa mimi ni mja tu. Hivyo basi niiteni mja wa Mwenyezi Mungu na Mjumbe wake” (1)
Na alikuwa akiomba
“Ewe Mwenyezi Mungu! usilifanye kaburi langu sanamu litaloabudiwa…” (2)
Mkufunzi mstaafu wa lugha ya kiarabu na masomo ya Kiislamu, marehemu Montgomery Watt, ameelezea katika kitabu chake, Muhammad ndani ya Makka:
“Utayari wake wa kupitia mateso kwa ajili ya imani yake, maadili mema ya wanaume na wanawake waliomuamini na kumuona kama kiongozi, na ukubwa wa mafanikio yake- yote yanadhihirisha uadilifu wake wa kimsingi. Kumdhania Muhammad kuwa tapeli kunazua matizo mengi zaidi kuliko kutatua”.(3)
Badala ya kutaka kuongezewa katika maisha ya dunia katika uhai wake au kutaka kuabudiwa huko mbeleni, Muhammad asingepata faida yoyote kwa kuwa na msismamo juu ya ujumbe wake- kitu ambacho ilibidi ateseke sana kwa ajili yake. Hata hivyo kuna uwezekano wa maelezo mengine. Alikuwa amechanganyikiwa au mwenda wazimu. Aliamini au alijiaminisha kwamba alikuwa anapata ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Labda hoja hii inaweza kuelezea msimamo wake katika upinzani. Tatizo ni kwamba ukweli uliopo pia haukubaliani na madai haya.
Je, alikuwa amechanganyikiwa?
Watu waliochanganyikiwa kawaida wanapata tabu katika kutofautisha ukweli na uongo. Wapo tayari kutumia ushahidi wowote ambao unaonekana unaweza kuunga mkono madai yao. Tukio moja muhimu linaloonyesha kwa umakini kwamba Mtume alikuwa na akili timamu na alikuwa mkweli muda wote, lilikuwa baada ya kifo cha mwanae mdogo wa kiume, Ibrahimu, chenye kuhuzunisha.
Ibrahim alifariki baada ya kuumwa kidogo na baada ya kuzikwa kulikuwa na kupatwa kwa jua. Baadhi ya Waislamu walidai kuwa huu ni ‘muujiza’ na wakaanza kusambaza habari hizi.
Habari zilisambaa kwamba jua lilipatwa kutokana na huzuni iliyosababishwa na kifo cha Ibrahimu. Aliposikia hayo Muhammad alijibu:
“Jua na mwezi ni alama za Mwenyezi Mungu havipatwi kwa ajili ya kifo au kuzaliwa kwa mtu yeyote. Kwenye kupatwa kwa jua/ mwezi, hivyo mkumbuke Mwenyezi Mungu na mgeukie kwa swala” (4)
Mtu aliyechanganyikiwa au mwenda wazimu angekubaliana na watu, haswa kwa sababu hii ilikuwa imani iliyotawala sana wakati huo:
“Ona! Huu ni ushahidi kwamba mimi ni Mtume, hata jua na mwezi vinajibu huzuni yangu!“
Hata leo pamoja na elimu ya kisayansi ya astronomia, watu wengi wangeweza kushawishika na hili! Hii pia ingekuwa hoja kama angekuwa muongo ambaye anajaribu kuwadanganya watu. Hata hivyo, mbali kabisa na madai ya kuwa amechanganyikiwa na anataka kujipa umuhimu, mazingatio ya Muhammad muda wote yalikuwa katika kuivuta mioyo ya watu irudi kwa Mwenyezi Mungu.
Wenda wazimu pia hudhihirika miongoni mwa watu wanaozungumza na kuwa na tabia zisizo na busara bila ya kuwa na msimamo. Wanaweza kudai kitu kimoja siku moja, na kuchukua msimamo mwingine kabisa wakati mwingine. Kitu kilichokuwa wazi kabisa toka mwanzo wa utume wake ni kutokubadilika kwa ujumbe wa Muhammad kwa zaidi ya miaka 20.
Ujumbe wake ulianza na kuendelea kwa uwazi, kwa kuwaita watu wamuabudu Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, huku akiwaonyesha watu jinsi mawazo yao yasivyokuwa na maana kwa kuabudu masanamu ambayo waliyatengeneza kwa mikono yao wenyewe, ambayo hayawezi kuwanufaisha wala kuwadhuru. Ukweli wa kwamba Muhammad aliweza kubadilisha tamaduni za muda mrefu zilizokuwa zimetawala miongoni mwa watu, inaonyesha kwamba asingeweza kama angekuwa amechanganyikiwa au mwenda wazimu.
Hata hivyo, Uislamu unaendelea hadi leo huku ukiendeleza na kubadilisha maisha ya watu. Cha kushangaza ni kwamba hata wana historia wasiokuwa waislamu wanamchukulia Muhammad kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa kuliko wote waliowahi kuishi. Hii ni kwa sababu ya athari ya mafundisho yake ambayo hayakudhibitiwa katika nyanja ya kiroho, na yanaweza kutumika kwa upana katika uwepo wa binadamu, ikiwemo uchumi, maisha ya familia, mfumo wa kisheria, mafunzo ya lishe na usafi.
Vipi na ilikuwaje mtu asiyeweza kusoma wala kuandika, aishiye katika jangwa, akaweza kuwa na elimu na ujuzi huu? Hakika, tunaweza kusema, anayesema mafunzo ya Muhammad ni kwa sababu alikuwa amechanganyikiwa, basi tunaweza kutumia kigezo gani kumtambua mtu mwenye akili timamu? Kwa mfano, alivyofanikiwa kukataza matumizi ya pombe. Hili lilikuwa jukumu gumu. Waarabu wa wakati ule walikuwa wanywaji sana wa pombe na mashairi mazuri sana yaliandikwa kuutukuza mvinyo.
Linganisha na jinsi jamii za kisasa, ambayo zinaujuzi na teknolojia za kisasa kama Marekani, na bado zimeshindwa kutekeleza ukatazaji wa unywaji wa pombe! Mbinu ya Muhammad ilikuwa yenye maono na umakini. Ilizingatia asili ya wanadamu na ulevi. Akawaondosha pole pole, kwa kuonyesha uovu na madhara yanayoweza kutokana na pombe, kisha kuwafanya waiache kwa hatua na mwishowe kuiacha moja kwa moja.
Aya za Qur’an zilipodhirishwa kuikataza pombe, watu waliokuwa wakinywa, wakazitupa pombe zao, wakazitema kutoka midomoni mwao na kuzimwaga mitaani, kutengeneza mito ya pombe iliyomwagwa. Zaidi ya hayo, yote haya yalifanywa kwa kujitolea bila shuruti!
Ishara nyingine ya utimamu wa Muhammad ulikuwa pale alipofanya makubaliano na maadui zake. Pengine mfano mzuri zaidi ni wa mkataba wa Hudaibia. Wafuasi wake walikuwa wanaelekea Makka kufanya hijja. Wapagani wakataka kuwasimamisha. Waislamu wangeweza kuingia Makka kwa urahisi na kuwashinda, lakini Muhammad aliamua kufanya mkataba! Qur’an ikauita mkataba huu ushindi mkubwa. Wafuasi wake wengi hawakuweza kulielewa hili.
Mmoja wa maswaha wake wa karibu kabisa alimuuliza wazi wazi na kumpa changamoto juu ya maamuzi yake. Hii ni kwa sababu masharti ya mkataba yalionekana kuwaonea waislamu. Muda mmoja wakati wa makubaliano, wakati mkataba ulikuwa unaandikwa, wapagani waliyafanyia mzaha matakwa ya Mtume kupewa cheo cha “Muhammad, mjumbe wa Mwenyezi Mungu” huku wakisema “Kama tungeamini hilo, basi kusingekuwa na ugomvi”.
Muhammad akawaomba waandishi wake waondoe cheo hicho na badala yake waandike “Muhammad- Mwana wa Abdullah”. Pale swahaba wake na rafiki yake wa karibu aliposhindwa kufuta cheo hicho, Muhammad akachukua kalamu na kufuta kwa mkono wake mwenyewe. Kufanya hivyo kwa upole haikuwa tabia ya wenda wazimu au watu waliochanganyikiwa.
Tena, yote haya yanaleta maswali: Muhammad alitoa wapi uelewa huu mkubwa, hekima na uelewa wa tabia za binadamu? Aliweza vipi kuleta mabadiliko haya makubwa, sio tu kwa watu wake, bali kwa dunia nzima?
Kama hakuwa muongo wala aliyechanganyikiwa basi alikuwa nani? Uwezekano mmoja umesalia. Ndio uwezekano pekee unaoweza kuelezea maajabu ya Muhammad.
Alikuwa mkweli.
Kama kweli alikuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliyepokea mwongozo kutoka kwa Muumba wake, basi inaelezea uaminifu wake, ukweli wake na msimamo wake usiotetereka katika kuwasilisha ujumbe wa kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja, pamoja na ujuzi wake wa kiundani juu ya hali za watu na uwezo wake wa kuwaongoza watu katika muongozo sahihi, hakika, watu wa mataifa na tamaduni mbalimbali mpka leo hii. Inaelezea undani wa kijamii, kisaikolojia, kitheolojia, kisheria, kihistoria na kiepistemiolojia, ndani ya mafunzo yake.
Mtume Muhammad alitumwa kurekebisha mahusiano kati ya binadamu na muumba wao. Aliwaita watu wamuabudu Mwenyezi Mungu mmoja peke yake. Mwenyezi Mungu mmoja ambaye hafanani na viumbe wake na ni mkamilifu, asiyeonekana, mwenye nguvu, mwingi wa upendo, mwingi wa rehma na mwingi wa kusamehe. Kuna ushahidi mmoja wa mwisho ambao tungependa kukupa katika kitabu hichi kuhimiza madai ya kwamba alikuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nao ni ukweli wa utabiri wake juu ya mambo ya mbeleni.
Kuna ushahidi mwingi wa hadithi za Mtume Muhammad na mwingi umetizamwa katika kitabu cha “Utabiri uliokatazwa”. Hapa tungependa kuzungumzia mmoja tu, kwa sababu utabiri huo umejitokeza kwa uwazi katika nyakati za karibuni.
Utabiri wa Waarabu Mabedui
Kutoka Milenia zilizopita, kuna Waarabu wa aina mbili: waishio mjini na “mabedui”. Wengi wao ni waishio mjini, ambao waliishi katika miji ya zamani kama Damaskas, Kairo, Makka, Sana’a na Baghdad. Mabedui walikuwa wafugaji. Walisafiri katika jangwa lililopana na walikuwa wakihama hama. Hata katika Zama za Dhahabu za Uislamu, pale Waarabu walipokuwa matajiri na wasomi wa dunia, mabedui walibaki katika hali yao ile ile waliokuwa nayo kwa maelfu ya miaka: maskini, wasio elimika na wakijitenga na dunia.
Katika nyakati za karibuni kama miaka ya 1940, Mchunguzi Muingereza, Bwana Wilfred Thesiger, alikuwa akisafiri katika maeneo ya Mabedui hawa na akaandika juu ya hali yao:
“Pindi niliposikiliza nkafikiria tena jinsi uwepo wa mabedui ulikuwa haujaimarika. Mwenendo wa maisha yao uliwafanya wawe waliokata tamaa na maisha; mambo mengi yalikuwa nje ya uwezo wao. Ilikuwa vigumu kwao kuandaa chakula cha siku iliyofuata kwa kuwa kila kitu kilitegemea mvua au wavamizi, magonjwa au lolote linginelo ambalo lingeweza kutokea lingeweza kuwaacha bila kitu, na kusitisha maisha yao. Walifanya waliyoweza, na hakuna watu wengine waliojitegemea zaidi yao, lakini vitu vilipokwenda mrama walikubali hatima yao bila kukasirika na kwa hadhi kama matakwa ya Mwenyezi Mungu.”(5)
Hata hivyo Muhammad alitabiri kwamba Waarabu Mabedui wa eneo lake siku moja wangekamilisha ujenzi wa majengo marefu:
“Sasa, niambie kuhusu saa ya mwisho”, aliuliza mtu huyo, Mtume akajibu, “Anayeulizwa hajui zaidi ya anayeuliza”
“Basi vipi kuhusu alama zake?” akasema mtu huyo.
Mtume akasema, “Pale utakapoona Mabedui waliopeku, bila nguo wakishindana katika kujenga majengo marefu.” (6)
Hizi ni miongoni mwa kauli za Mtume Muhammad ambazo ni maarufu zaidi na zilizothibitishwa.
Pale Muhammad alipoulizwa kuhusu “saa ya mwisho”, akimaanisha kukaribia kwa siku ya kiyama, zingatia jibu lenye undani alilolitoa: watu maalumu, Waarabu maskini, Mabedui wa eneo hilo walitajwa.
Muhammad angeweza kutafuta usalama kwa kutumia maneno ya ujumla kama ” utaona mashindano katika ujenzi wa majengo marefu…” ambayo ingeweza kutumika kwa mtu yeyote duniani.
Katika rasi ya Uarabuni leo, tunakuta kwamba baadhi ya makundi ya Waarabu ambao walikuwa mafugaji wa ngamia na kondoo, masikini mpaka kati ya karne ya ishirini, sasa wanashindana katika kujenga majengo marefu. Mabadiliko haya yalitokea vipi mara moja? Watu maskini kuliko wote duniani, ambao walivaa matambara, baadhi yao wakishindwa hata kumiliki viatu, waliwezaje kuwa watu matajiri kuliko wote duniani?
Hakika, msururu wa matokeo uliwezesha hili kutokea: Kuanguka kwa dola ya Ottoman (Ambayo ilikuwa ikitawala rasi ya Uarabuni), kufuata Uislamu waliofuata sheria ulioungwa mkono na viongozi wa Mabedui na kuondoa waangalizi wa zamani wa Kihashim wa misikiti mitukufu ya Makka na Madina.
Kitu kingine kiliwezesha mabadiliko haya ya haraka. Kitu ambacho dunia ya sasa inakitegemea sana, pengine zaidi ya kitu kingine chochote; Mafuta! Majangwa ya Mabedui ambayo yalionekana matupu yana mafuta ya kutosha. Mabedui wakavuka kutoka kutumia ngamia na sasa kutumia magari ya kifahari ndani ya kizazi kimoja! Leo, majengo marefu kuliko yote yanapatikana kwa wingi katika rasi ya Uarabuni kuliko pengine kokote duniani, zaidi katika maeneo ya makazi ya Mabedui. Burj Khalifa, jengo lipatikanalo Dubai ndio jengo refu kuliko yote duniani lenye urefu wa mita 828.
Muda mfupi baada ya kukamilika, familia ya kipinzani kutoka Saudi Arabia ilitangaza kwamba itajenga jengo refu zaidi yake (mita 1000) – Jengo la Ufalme- wanashindana miongoni mwao juu ya nani atajenga jengo refu kuliko yote duniani. Kitu gani kilimfanya Muhammad afanye utabiri huu?
Kama angebuni utabiri huu, ingeleta maana zaidi kama angehusisha utabiri huu na mataifa yaliokuwa na nguvu wakati ule: Warumi, Persia, hata China (ambao sio kama Waarabu) walikuwa tayari na tabia ya kujenga majengo ya kifahari na majumba ya wafalme. Mtume Muhammad mwenyewe hakutaka Waislamu wajihusishe na utajiri usio wa lazima. Hakika alionya juu ya madhara yake na jinsi unavyoweza kuleta ufisadi katika umma wake.
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba hakupenda kuhamasisha kujenga majengo! Alikuwa mtu wa kawaida aliyeishi kwenye nyumba ya kawaida na alitaka waislamu wengine waishi maisha ya kawaida. Hivyo ndivyo alivyofundisha na alivyoishi. Kama angetaka utabiri huu uwe kweli basi angewahamasisha Waarabu wajenge majengo marefu na labda angeanza kufanya hivyo yeye mwenyewe! Hakika utabiri huu sio wa uongo.
Muhammad, rehma na amani ziwe juu yake, alijuzwa sehemu ya yatakayokuja mbeleni na Mwenyezi Mungu. Alikuwa akiwaonya binadamu juu ya kuja kwa siku za mwisho. Tupo ndani ya siku hizo sasa.
Hakuna miongoni mwetu ambaye ataishi milele! Muda wetu sote umekaribia. Hakika muda unakwisha.
Kujiandaa
Kuna mtu alimuuliza Mtume kuhusu siku ya mwisho,
“Siku ya mwisho itakuwa lini ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?” Mtume akasema, “Umeandaa nini kwa ajili yake?” Mtu huyo akasema, “Sijaandaa sala nyingi wala funga wala sadaka, lakini nampenda Mwenyezi Mungu na mjumbe wake” Mtume akasema, “Utakuwa na umpendaye” (7)
Tunachojifunza kutokana na hili ni kwamba kama tunampenda Mwenezi Mungu na Mtume wake wa mwisho, tutaongoka. Hakika mapenzi ya kweli sio tu imani bali pia matendo. Lazima tujitahidi kumfuata mtume wa mwisho ili kupata uongofu.
Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana. Qur’an surah ya 33, ayah ya 21
Kitabu hicho sio kwa ajili ya majaribio ya kifikra tu. Kama unaamini kwamba Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) alikuwa mkweli basi ujumbe aliokuja nao pia ulikuwa wa kweli na itabidi uukubali kwa moyo wako wote ili uweze kujua kusudi la maisha haya na upate ufaulu katika maisha yafuatayo.
Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu. Sema: Mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri. Qur’an Surah 3, ayah 31-32 .
Marejeo:
[1]Imetolewa kwenye sahih Bukhari. [2] Tahdheer al-Saajid min Ittikhaadh al-QuboorMasaajid, uk. 24-26.
[3] Watt, W. M. (1953) Muhammad at Mecca. Oxford:Oxford University Press, uk. 52.
[4] Imetolewa kwenye sahih Bukhari. [5] Thesiger, Wilfred (2007), Arabian Sand, Penguin,Kindle Edition, Loc 3572.
[6] Imetolewa kwenye sahih Muslim. [7] Imetolewa kwenye sahih Bukhari.